Nishow Beshte Yako, Nikushow We Ni Nani | YADA Group


Kamwe hawakukosea wahenga waliponena, ‘akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki.’ Marafiki wema huwa na ushawishi mkubwa juu ya matendo yetu hasa katika siku za ujana wetu. Mawazo, mienendo na maamuzi tunayoyafanya mara nyingi hudhihirika kupitia wale wanaotuzunguka.


Abdul alipohitimu masomo yake ya kidato cha nne na kurudi kwao nyumbani, alijihisi mpweke mara nyingi kwa kuwakosa marafiki aliosoma nao sababu baada ya masomo ya shule ya upili ilibidi kila mmoja kurejea nyumbani kwao ili kusubiri matokeo ya mtihani na kisha kujiunga na chuo kikuu. Kipindi hicho Abdul aliyaona maisha kuwa magumu kwa sababu nyumbani ufukara ulikua umewagubika asione ni kipi anachoweza kujishughulisha nacho. Ilimbidi kutulia nyumbani siku hizo zote huku wazazi wake wakiondoka kila alfajiri kwenda kujishughulisha na kazi za sulubu angalau wapate riziki ya kila siku.


Mawazo yalizidi kumsonga Abdul kwani hata baada ya kupata matokeo bora hakuwa na tumaini la kuendeleza masomo yake kutokana na hali duni ya maisha iliyowaandama nyumbani. Alitamani angekuwa na marafiki wake wa shuleni ili kuzungumza nao apate ushauri kutoka kwao lakini hakuwa na namna yoyote ya kuwasiliana nao maadam hata rununu hakuwa nayo.


Mambo yalivyozidi kuwa magumu, Abdul aliamua kufanya urafiki na vijana wenzake mtaani kwao. Kundi hili la vijana lililokuwa mtaani kwao siku zote halikujihusisha na shughuli yoyote yenye faida ila uvutaji bangi na madawa mengine ya kulevya. Muda si muda Abdul naye alitumbukia katika jaribu hilo naye akaanza kulangua mihadarati kama vijana wale wa mtaa.Urafiki huu mbovu uliendelea na baada ya kipindi kifupi Abdul alianza kushiriki uhalifu ambapo Pamoja na marafiki wale waliwashambulia wakaazi wa eneo lao, kuwapora mali na kujeruhi baadhi yao.


Walinda usalama walipopata taarifa kuhusu kundi hilo la uhalifu lililowahangaisha wakaazi, walianzisha msako na kuwakamata vijana wale akiwemo Abdul ambaye alijutia sana kujiunga na kundi lile.


Matukio haya yalikua ni funzo kwa Abdul kuwa marafiki wabaya huibua mikosi na balaa kwa maisha ya mtu. Aligundua bila shaka kuwa kutembea na rafiki mwema gizani ni bora kuliko kutembea naye mwangani. Aliwazia na kuwakumbuka marafiki wake shuleni ambao walishiriki mambo mengi mazuri Pamoja ila hakujua afanyaje ili wawe pamoja kwani masomo ya shule ya upili walikua tayari wamekamilisha.


Baada ya kuwachiliwa kutoka gerezani, Abdul alifanya maamuzi kutojiunga na kundi lile la uhalifu tena. Alitumia mda wake mwingi kufanya ukulima mdogo pale nyumbani na ufugaji wa kuku jambo ambalo alishauriwa kufanya na rafiki mmoja aliyejulikana kama Musa kutoka mtaa jirani. Shughli hizi za ukulima zilimpa mapato mazuri kwani aliuza kuku na mboga kwa majirani jambo ambalo lilibadilisha hali yao pale nyumbani na likawapa wazazi wake furaha si haba. Isitoshe, mapato yale yalimwezesha kurudi shule na kupelekea wazazi wake kuwacha kung’ang’ana na shughuli zile za sulubu na kurudi nyumbani kuendeleza kilimo biashara ile.


Abdul aliishikumpenda rafiki yake Musa na kutamani kuwa angemfahamu mapema kabla ya kujiunga na genge lile la uhalifu.


Kuwa na marafiki wazuri wanaokuthamini siku zote huibua matokeo mazuri. Kwao utapata ushauri utakaokufaa, maonyo dhidi ya uovu na pia ushawishi mzuri utakaokusaidia kufanya maamuzi bora kwa maeneo mbalimbali kimaisha.


Sharti vijana kufanya urafiki na watu wanaoleta faida katika maisha yao. Vijana wengi wamejipata mashakani kwa kujihusisha na marafiki wenye mienendo isiyofaa kuigwa na jamii. Kabla ya kufanya urafiki na mtu yeyote, ni muhimu kuchunguza mienendo na maneno ayazungumzayo mtu ikiwa yanajenga ama yanabomoa. Elewa kwamba, rafiki mwema ni yule anayekushauri na kukuelekeza kwa njia zinazofaa. Vilevile, rafiki anayekuthamini ni yule anayekuonya dhidi ya kuchukua mwelekeo usiofaa. Thamini rafiki mwema!!